Monday 30 March 2015

MKE WA GWAJIMA AIBUA HOFU KUHUSU AFYA YA MUMEWE

Familia ya Kiongozi wa Kanisa la Ufunuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, imeeleza hofu yake  kwamba imeshangwazwa na hali ya afya ya kiongozi huyo kubadilika ghafla akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi akihojiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, mke wa Askofu Gwajima, Grace Gwajima, alisema familia bado haielewi ni kwa namna gani Askofu huyo alizimia ghafla wakati aliondoka nyumbani akiwa mzima wa afya.
Alisema kama familia kuna vitu vinavyowachanganya na hawapati majibu haraka ikiwamo la Askofu Gwajima kuondoka nyumbani akiwa mzima wa afya huku akitembea, lakini muda mfupi baadaye anapelekwa hospitali akiwa amezimia akihojiwa na polisi.
“Tunahisi kuna kitu amefanyiwa, kwa maana haiwezekani mtu aondoke nyumbani akiwa wa afya, lakini baadaye kidogo tunapewa taarifa amezimia yupo TMJ, hapa kutakuwa na kitu,” alisema Grace akiwa na mmoja walinzi wa Askofu Gwajima.
HALI YA ASKOFU GWAJIMA
Akizungumzia hali ya Askofu Gwajima, aliyelazwa hospitalini hapo kwa siku tatu, Grace alisema mumewe anaendelea vizuri na madaktari walikuwa wanajiandaa kumtoa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) jana na kumpeleka wodi ya wagonjwa wa kawaida.
Alisema kwa sasa Askofu Gwajima anaweza kuongea, kula chakula na hata kuzungumza na watu mbalimbali wanaofika kumjulia hali. “Kuna improvement zimeaza kujitokeza, ki ukweli kuna hali ya uzima na anaendelea vizuri,” alisema Grace.
Hata hivyo, waandishi wa habari walizuiwa  na uongozi wa Hospitali ya TMJ kwenda kumwona Askofu Gwajima na badala yake walimwita Grace azungumze na waandishi.
KUKAMATWA KWA WACHUNGAJI
Mke wa Askofu Gwajima (Grace), alidai kuwa juzi usiku Polisi walifika hospitalini hapo na kuwakamata wachungaji 30 waliofika kumjulia hali Askofu Gwajima.
Alidai kuwa Polisi waliwakamata wachungaji hao pamoja na magari yao na kuwapeleka kusikojulikana.
“Jana usiku kulizuka tafrani hapa hospitalini, Polisi walifika na kuwakamata wachungaji wapatao 30 wa Kanisa la Ufufuo na Uzima na kuondoka nao,” alidai Grace.
Hata hivyo, NIPASHE lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kuthibitisha taarifa hizo, lakini alisema angetuma taarifa hiyo kwa vyombo vya habari. Hata  hivyo, hadi tunakwenda mitamboni Kova hakutuma taarifa hiyo.
ULINZI WAIMARISHWA HOSPITALINI
Hali ya ulinzi katika Hospitali ya TMJ iliimarishwa ndani na nje ya eneo hilo, kwa kuwapo kwa askari waliovalia nguo za kiraia.
Askari hao walionekana wakiimarisha doria nje ya wodi aliyolazwa Askofu huyo na kuzuia watu kusogelea wodi hiyo.
Nje ya hospitali hiyo kulikuwapo na gari la Polisi lililokuwa limeegeshwa likiwa na askari waliovalia nguo za kiraia, huku wengine wakiingia ndani na kutoka kila mara.
Mbali na askari hao, pia walinzi wa Askofu Gwajima nao walionekana wakiwa karibu na wodi hiyo.
Ijumaa iliyopita, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilimhoji Askofu Gwajima kwa tuhuma za kumkashifu na kumtukana hadharani Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Policarp Kardinali Pengo.
Muda mfupi wakati wa mahojiano hayo yakiendelea, Askofu Gwajima alizimia ghafla akiwa kwenye chumba cha mahojiano katika Kituo cha Polisi Kati.
Kufuatia hali hiyo, Askofu huyo alipelekwa katika hospitali tofauti ikiwamo ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na mwishowe kupelekwa TMJ

NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...


aziz bilal09:46




Hii tabia ya kuwakamata viongozi wa dini sijui itaisha lini nchini Tanzania,police wapunguze maonezi dhidi ya viongozi wa kiroho.

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!